Alhamisi , 28th Apr , 2016

Halmashauri ya wilaya ya Mtwara pamoja na manispaa ya Mtwara Mikindani zimepitisha mpango wa matumizi ya ardhi utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka 20, ambapo yametengwa maeneo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Rashidi Mtima,

Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao cha kupitisha mpango huo, kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Rashidi Mtima, amesema mpango huo ndio utakuwa nguzo ya kisheria katika matumizi ya ardhi katika halmashauri hizo huku ukilenga kuhakikisha kuwa Mtwara inahudumia shughuli za gesi.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Zacharia Nachoa, amesema katika uendelezaji wa mpango huo, kila halmashauri itakuwa na wajibu wa kuona yale yaliopo katika mpango yanatekelezwa, jambo ambalo litasaidia kuondoa ujenzi holela.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, amewahamasisha wananchi kuutambua na kuupokea mradi huo ambao anaamini utawanufaisha kupitia ardhi zao iwapo watazitunza vizuri na kuacha kuwauzia watu kwa ghara za chini ambazo hazitakuwa na tija kwao.

Maeneo mengine yaliyotengwa kupitia mpango huo ni eneo la Naumbu lililotengwa kwa ajili ya Viwanda, Mjimwema ambako huko ni kwa ajili ya elimu ya juu, Nanguruwe kumetengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo na makazi pamoja na eneo la Mtwara mjini lililotengwa kwa ajili ya shughuli za kibiashara.

Sauti ya kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Rashidi Mtima,
Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally,