Jumanne , 16th Mei , 2017

Mbunge wa jimbo la Temeke Abdallah Mtolea (CUF) amefunguka na kuwataka Wabunge kutojisahaulisha miundombinu ya elimu Tanzania kuwa siyo rafiki kwa wanafunzi wa kike, hivyo watumie busara kufanya maamuzi kuhusu wanaopata Mimba wakiwa shuleni.

Jana wakati akichangia hoja bungeni kwenye wizara ya Elimu kuhusu wanafunzi wanaopata mimba kurudi shuleni, Mhe. Mtolea amewataka wabunge kutoshabikia suala la mabinti kunyimwa haki ya masomo kwani siyo wote wanaojitakia kubeba mimba lakini mazingira ya vishawishi ndiyo chanzo kwa wanafunzi wengi kuishia njiani kwa kubeba mimba.

"Wabunge msimalize maneno kwa kuwa watoto wenu wanasoma katika shule nzuri, tukumbuke watanzania wengi watoto wetu wanasoma shule zenye umbali mrefu kufika, hebu tusiwe wageni wa nchi hii, hosteli ni chache za kuhifadhi mabinti wote sasa fikiria mwanafunzi anapewa lifti mwaka mzima ya boda boda ataweza kukwepa vishawishi? hata nyie na ubunge wenu ndni ya siku thelethini mnaweza kuingia kwenye mahusiano je mwanafunzi?

Pamoja na hayo Mhe. Mtolea amesisitiza huruma itumike katika maamuzi, huku akiwahoji wabunge wanaopinga wanafunzi waliopata tatizo la ujauzito shuleni, kati ya waathirika wa dawa za kulevya na waliopata mimba ni wapi wamefanya makosa ya kukusudia?

"Juzi serikali imetenga mamilioni ya hela kwa ajili ya kujenga vituo vya kuwapatia msaada vijana walioathirika na dawa za kulevya kwa madai ya kujifunza, sasa kwa nini hawa mabinti wasipewe nafasi ya kujifunza kutokana na makosa maana asilimia kubwa ni wale walioshawishiwa kutokana na mazingira na wengine ni wale wa matukio ya ubakaji? hata Waziri mwenye dhamana anajua tatizo kubwa linatokana na nini"- Mh. Mtolea aliongeza.

Pamoja na hayo Mtolea ameongeza kwa kuwashukia wanaopinga wanafunzi wasirudi shuleni wao ndio wanaweza wakawa chanzo cha mimba mashule.