Ijumaa , 3rd Jun , 2016

Rais Dkt.John Magufuli pia amewataka wanafunzi wa vyuo nchini kuacha kujihusisha na masuala ya siasa na badala yake wazingatie jukumu kuu lililowapeleka vyuoni huku akibainisha kuwa serikali haitavumilia vitendo vya vurugu vyuoni.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia mamia ya jamii ya wanachuo

Rais Magufuli ametoa kauli jana wakati akizungumza na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho inayojengwa katika kampasi ya Mlimani upande wa mashariki mwa chuo.

Akiwahutubia maelfu ya wanajumuiya hiyo wanaojumuisha wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi wa chuo, Dkt. Magufuli amesema serikali yake imedhamiria kutoa elimu bora kwa watanzania na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto mbalimbali zinazovikabili vyuo.

Amewaahidi kuwa serikali yake itahakikisha inatoa mahitaji ya wanafunzi ikiwemo mikopo na kuboresha miundombinu ya vyuo, lakini amewataka wanavyuo nao kuwa wavumilivu na wazalendo pale ambapo mahitaji hayo yatachelewa kutokana na mchakato wa kuyapata kuhitaji muda.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho ambaye ni Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemuomba Rais Magufuli asaidie kuboresha miundombinu ya chuo hicho ikiwemo ujenzi wa mabweni ya wanafunzi ambao kwa takribani asilimia 70 wanaishi nje ya chuo,

Uzinduzi wa ujenzi wa Maktaba hiyo ya kisasa umehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing ambaye nchi yake ndio imetoa msaada wa dola za Marekani zaidi ya Milioni 41 kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba hiyo.

Sauti ya Rais Dkt.John Magufuli akiwataka wanafunzi kutojihusisha na Siasa