Jumamosi , 27th Aug , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo ni wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM) ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye mpango huo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa Nairobi nchini Kenya

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Agosti 26, 2016) wakati akichangia mada katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya InterContinental jijini Nairobi, Kenya.

“Nitumie fursa hii kukiarifu kikao chako kwamba Tanzania imeshaanza kutekeleza mpango kazi wa Kitaifa ambao umejikita kutatua changamoto katika sekta za maji, elimu, kilimo, nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa kwenye kikao cha APRM,” alisema.

“Ili kuhakikisha kuwa zinafanyiwa kazi haraka, changamoto hizi za kisekta zimepewa kipaumbele kwenye Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016-2021 ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,” aliongeza.

Tanzania ilifanyiwa tathmini yake Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Mapema, akifungua mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema viongozi wa Afrika hawana budi kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani wa kibiashara.

Alisema nchi wanachama wa mpango huo hawana budi kujenga umoja kama njia ya muafaka ya kufikia makubaliano hayo.