Jumatatu , 18th Sep , 2023

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) Maharage Chande amekanusha uwepo wa mgao wa umeme kama ambavyo kumekuwa na taarifa mitandaoni kuwa kwa sasa kuna mgao wa umeme unaopelekea baadhi ya maeneo kukosa huduma hiyo.

Maharage Chande akizungumza katika kipindi cha Supa Breakfast kinachorushwa na East Africa Radio amesema katika mifumo ya umeme hitilafu lazima zitokee na pale zinapotokea haimaanishi nchi nzima umeme unakosekana bali unatokea upungufu ambao hupelekea baadhi ya maeneo kukosa umeme.

"Huwezi kusema utakuwa na mtandao wa umeme isitokee hitilafu na pale zinapotokea wateja wetu huwa wanafahamishwa lakini pale ambapo tunapata upungufu siyo kwamba nchi nzima hakuna umeme, kuna baadhi ya meeneo yanakosa na pia tunatoa taarifa kwenye hayo maeneo na tutaendelea kufanya hivyo" alisema Maharage Chande.

Bwana Chande pia amekiri kuwepo kwa matatizo katika mifumo ya umeme ambayo inahitaji muda ili iweze kurekebishwa na kuendelea kuzalisha nishati hiyo kwa uhakika na ufanisi zaidi kwani tayari kuna mipango mizuri ambayo inaendelea kwaajili ya kushugulikia matatizo hayo.

"Kweli tuna matatizo lakini yanahitaji muda kutatuliwa hakuna jinsi ya kufanya kwa haraka zaidi ya hivyo ilivyoelezwa lakini uzuri ni kwamba mipango mizuri ipo na utekelezaji unaenda vizuri" - Maharage Chande

Amesema kwa sasa wananchi na wateja wa TANESCO wanapaswa kuwa watulivu na kuendelea kusubiri tatizo likiwa linaendelea kupatiwa ufumbuzi huku akisema jitihaada zinafanywa na wizara pamoja na serikali licha ya kuwa ni kipndi kigumu kuvumilika.

"Wateja na wananchi watuvumilie katika kipindi hiki najua ni kigumu kuvumilika na kuelekeweka lakini wafanyakazi wanajitahidi, wizara inajitahidi na serikali inajitahidi kuhakikisha tunatatua changamoto, vile vile uchumi unakua sana kwahiyo ni vizuri na mahitaji ya umeme yanaongezeka kwahiyo tuko katika kushindana kuzalisha na matumizi ambayo ni mashindano mazuri kwa ustawi wa nchi yetu" Maharage Chande.

"Hii sekta ya umeme ni safari na safari ni hatua, Bwawa la mwalimu Nyerere ni hatua kubwa katika safari hii na baada ya bwawa hilo vyazo vingine bado vinaendelea kusanifiwa navyo pia vitajengwa, kuna umeme wa upepo SIngida, umeme wa jua Shinyanga, kuna umeme wa Joto ardhi kwahiyo kuna safari ambayo inaenda na hatua kwa hatua na Mwalimu Nyerere ni moja ya hatua" aliongeza Maharage Chande

Akizungumzia kuhusu jitihada ambazo serikali inazichukua kukabilina na mabadiliko ya tabia nchi kwenye uzalishaji wa nishati ya umeme, Bw. Maharage Chande amesema kwa sasa serikali inajenga kituo cha uememe wa jua pale Kishapu Shinyanga, kumalizia usanifu wa kituo cha umeme wa upepo Makambako pamoja na Singida.

"Tunatakiwa kufahamu katika uwekezaji wa umeme kabla haujaijenga lazima ufanye usanifu na upembuzi yakinifu na upembuzi  yakinifu ambao peke yake hiyo ni kazi siyo ya miezi 12 bada ya hapo kutafuta sekta miezi nane kwahiyo jumla miezi 20 halafu uanze kujenga kama ni jua na upepo unaweza kutumia miezi 15 mpaka 18 kujenga kama ni gesi 36 kama maji miezi 60" Bw. Chande.