Alhamisi , 24th Nov , 2022

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt.Alphonce Chandika, leo amekutana na mabalozi wa Tanzania waliopo Mashariki ya kati, Ulaya na Amerika, Asia kwa dhumuni la kuwaeleza mafanikio yaliyo letwa na Serikali katika sekta ya afya.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt.Alphonce Chandika

Dkt. Chandika amesema kuwa "Serikali imewekeza pesa nyingi kwa kuweka majengo mazuri, vifaa tiba vya kisasa na rasilimali watu, hivyo nasi tunatoa huduma kwa viwango hivyo hivyo, tokea Hospitali ianzishwe mahusiano baina ya Hospitali na nchi za nje yamekuwa yakiimarika siku kwa siku"

Kwa upande wake Mhe. Balozi Dkt Asha Rose Migiro, ameipongeza Hospitali kwa kuwa imekuwa ikitoa huduma zinazoendana na teknolojia ya sasa tena kwakuzingatia huduma kwa mteja. 

"Ukifika Hospitali ya Benjamin Mkapa huitaji kujitambulisha ili upate huduma nzuri maana utahudumiwa kwa kiwango kizuri pasipo kujali wadhifa wako kwakweli mnastahili pongezi kubwa, endeleeni na moyo huo wa kuwahudumia wananchi pasipo kubagua" amesema Dr Migiro, ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

Aidha Mhe. Balozi Swaiba Mndeme ameeleza nimuhimu kuzisaidia Taasisi zetu hususani Hospitali, "Tunaposaidia hizi Hospitali tunakuwa tumewafikia wananchi moja kwa moja nasi shabaha yetu iwe ni kuwasidia wananchi kwa kuiunganisha BMH na wataalamu walipo kwenye nchi tulizopo".

Hospitali ya Benjamin Mkapa ilizinduliwa Oktoba 13, 2015, na tangu izinduliwe imekuwa ikikuwa kwa kasi kubwa huku ikitoa huduma zake kwa ubunifu wa hali ya juu.