Jumanne , 16th Feb , 2016

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako leo amewasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini Tanzania (HESLB) George Nyatega na wakurugenzi watatu.

Wakurugenzi hao wengine waliosimamishwa ni pamoja na Yusufu Kisare ambaye alikuwa mkurugenzi wa fedha na utawala, Juma Chagonja Mkurugenzi wa urejeshaji mikopo na Onesmo Laizer Mkurugenzi wa upangaji na utoaji mikopo.

Akitangaza kusimamishwa kazi kwa watendaji hao waziri Profesa Ndalichako amesema amechukua uamuzi huo baada ya kubaini ucheleweshaji wa makusudi wa mikopo pamoja na ubadhirifu wa fedha.

Waziri amebainisha makosa mengine kuwa ni pamoja na udhaifu wa kiutendaji , malipo yasiyo sahihi pamoja na udhaifu katika mifuko ya fedha, huku wizara ikichukizwa na migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa uzembe unaofanywa na watendaji hao katika kuwahudumia kwa wakati.