Alhamisi , 5th Mar , 2015

Hakimu mkazi wa mahakama ya Mkoa wa Dodoma Rebecca Mbilu amemtaka mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabishara nchini, Johnson Minja kuwaambia wafanya biashara nchini waache kufunga maduka yao wakati wa kesi yake kwani ni sharti mojawapo la dhamana yake.

Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama vya Wafanyabiashara Nchini, Bw. Jonson Minja (mwenye koti) akisomewa mashtaka yake katika mahakama ya mkoa wa Dodoma

Hakimu Mbilu ameyasema hayo leo wakati wa kesi inayomkabili mwenyekiti huyo kufuatia wafanyabiashara nchini kufunga maduka yao kwa ajili ya kuja mkoani Dodoma kusikiliza kesi inayomkabili mwenyekiti huyo.

Wakati wa kusikiliza kesi hiyo ambayo imepangwa kutajwa tena Machi 26 mwaka huu, Mbilu amemwambia Minja awaambie wafanyabiashara kufungua maduka yao wakati kesi hiyo ikiwa inaendelea mahakamani.

“Moja ya sharti la dhamana yako ni kuhakikisha kuwa unaendeleza amani wakati wote wa kesi yako ikiwa ni pamoja na kuwaambia wafanyabiashara waendelee kufungua maduka yao ili wananchi waendelee kupata huduma, kwanini umewaambia wafanya biashara wafunge maduka yao?” alihoji hakimu Mbilu.

Hata hivyo Minja amejibu kwa kifupi kuwa hana taarifa zozote za wafanyabiashara nchini kufunga maduka.

Naye wakili wa Mshtakiwa huyo, Godfrey wasonga amesema mahakamani hapo kuwa wafanyabiashara walikuja kusikiliza kesi hiyo siyo kwamba wamefunga maduka yao bali walikuwa wamekuja mkoani Dodoma kwa ajili ya matembezi yao wakati maduka yao yakiendelea kutoa huduma.

Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida wafanyabiashara hao wamemhakikishia hakimu huyo kuwa wamefunga maduka yao nchi nzima kwa ajili ya kuja kusikiliza kesi inayomkabili mwenyekiti wao kwani kesi hiyo siyo ya kwake peke yake bali ni ya wafanyabishara wote Tanzania.

“Unasikia Minja kama wafanyabishara wataendelea kufunga maduka yao wakati wa kesi yako na kusababisha wananchi kukosa huduma nitakufutia dhamana na utakwenda kulala Isanga,” alisema Hakimu Mbilu.

Awali mwendesha mashtaka wa serikali, Godfrey Wambali ameiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi MAchi 26 kwa kuwa uchunguzi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Mwenyekiti huyo anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuwachochea wafanyabiashara mkoani Dodoma kutenda kosa na kuwakataza wafanyabiashara nchini wasitumie mashine za kieletroniki za kukusanya kodi za efds ambavyo vyote ni makosa ya jinai.