Mkuu wa mkoa wa Songwe, Luteni Mstaafu Chiku Galawa.
Katika Zoezi la Uhakiki wa watumishi hewa lililofanyika mapema mwezi Machi mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli wilaya nne za mkoa wa Songwe ziliambatanishwa na zile za mkoa wa Mbeya kuhakikiwa kwa kuwa mkuu wa mkoa huo mpya Luteni mstaafu Chiku Galawa alikuwa hajawasili mkoani mwake.
Kufuatia uhakiki huo, watumishi 32 kutoka halmashauri za Mbozi,Tunduma, Momba na Ileje walibainika kuwa hewa ambapo walikuwa wameiingizia serikali hasara ya jumla ya shilingi 141,994,061 kwa malipo ya mishahara.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa huo wa Songwe Luten Mstaafu Chiku Galawa alisema baada ya kufika mkoani hapa alitoa muda wa mwezi mmoja kwa maafisa utumishi kurejesha fedha hizo.
Alisema hadi jana( Mei 10) fedha zilizokuwa zimerejeshwa ni shilingi 55,632,929 hivyo kiasi kilichosalia kwa halmashauri hizo ni shilingi 86,361,381.
Alisema kwa halmashauri ya wilaya ya Mbozi iliyosababisha hasara ya shilingi 69,073,315.20 kutokana na kuwa na watumishi hewa 10 imekwisharejesha kiasi cha shilingi 28,734,784 hivyo bado shilingi 40,338,534.
Halmashauri ya wilaya ya Momba iliyokuwa na watumishi hewa11 ilikuwa na hasara ya shilingi 34,409,381 imerejesha shilingi 6,707,740 bado shilingi 27,701,641 na halmashauri ya wilaya ya Ileje iliyokuwa na watumishi hewa sita ilikuwa na hasara ya shilingi 22,891,610,imerejesha shilingi 20,190,404.71 bado shilingi 2,201,205.63.
Kwa Halmashauri ya mji wa Tunduma iliyokuwa na watumishi hewa watano ilisababisha hasara ya shilingi 15,620,000 na haijarejesha kiasi chochote cha fedha.
Galawa alisema bado hajafahamu iwapo fedha zinazorejeshwa zinatoka katika mifuko binafsi ya maafisa utumishi, bali inapobidi itawalazimu kufanya hivyo kwakuwa lazima fedha za serikali zirejeshwe zote katika muda alioagiza.
Alisema taarifa alizonazo ni kuwa zipo baadhi ya fedha zilizokutwa kwenye akaunti za watumishi ambao ni marehemu,waliacha kazi au kustaafu waliokuwa wakiendelea kulipwa mishahara lakini hawakuchukua fedha hizo benki.