Jumatano , 14th Feb , 2024

Serikali imeweka wazi kuwa itaendelea kutatua migogoro mbalimbali ya Sekta ya Maliasili na Utalii ikiwemo iliyo katika maeneo ya hifadhi kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi kwa ujumla.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema hayo Februari 14,2024 katika kikao kati yake na Wabunge wa Mikoa ya Shinyanga na Tabora kilichofanyika jijini Dodoma, kwa lengo la kusikiliza changamoto zilizopo kwenye majimbo yao.

Amefafanua kuwa si vema kwa Serikali kuendelea kuwa na migogoro ya hifadhi kwa kipindi kirefu na si afya kwa Taifa, hivyo Serikali itafanya jitihada za kuitatua.

Kufuatia hatua hiyo, amewaelekeza Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii na  Taasisi zake kufanya tathmini ya kina kuhusu migogoro iliyopo katika maeneo yao na kuangalia namna bora ya kuitatua.

Kuhusu uadilifu wa Watendaji na Askari Uhifadhi, Waziri Kairuki amefafanua kuwa Serikali itaendelea kutoa mafunzo zaidi na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa uadilifu na kuwapatia vitendea kazi ili waweze kujua wanatakiwa kufanya nini kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), baadhi ya  Wabunge wa Mikoa ya Shinyanga na Tabora, Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake za Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)  na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).