Alhamisi , 28th Mei , 2015

Mgogoro ulioibuka hivi karibuni baina ya wananchi na muwekezaji wa Shamba la Kahawa la Burka katika Kijiji cha Olasiva Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, umeendelea kuchukua sura mpya baada ya kubainika kwa maslahi ya kisiasa yanayochochea mgogoro huo.

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Hasna Mwilima

Mgogoro huo umeibuka kufuatia baadhi ya wananchi wa eneo hilo kulalamikia utaratibu wa kuingia katika shamba hilo kubwa la kahawa kwa shughuli za kuokota kuni na kukata majani kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.

Siku kadhaa zilizopita wananchi wa Kijiji cha Olasiva kupitia katika mikutano ya kijiji iliyowajumuisha pia viongozi wa vijiji na kata, walilamikia hatua ya muwekezaji wa shamba la Burka Coffee Estate lililopo Nje Kidogo ya Jiji la Arusha, wakimtuhumu kwa kushindwa kwake kuonyesha ushirikiano na wananchi wa kijiji kinachozunguka eneo lake..

Kufuatia sakata hilo,kituo hiki kimelazimika kufika katika eneo la shamba la Kahawa la Burka na kukuta shughuli za kukata majani na kuokota kuni zikiendelea huku baadhi ya wananchi wakitumia njia inayokatiza shambani hapo kwa utaratibu maalumu unaotajwa kuwekwa kwa sababu za kiusalama..

Kwa upande wake Meneja wa Shamba la Burka Coffee Estate Hunter Flint amesema kwa kuzingatia dhana ya mahusiano na wanajamii uongozi wa shamba hilo ulilazimika kuruhusu wananchi kuokota kuni na kukata majani kwaajili ya mifugo, lakini wameamua kuweka utaratibu maalumu wa kuwahoji watu ili kuondoa hatari ya kuruusu wale wenye nia ovu kuingia ndani ya eneo hilo la uwekezaji hatua ambayo imezua malalamiko na vitisho dhidi ya kampuni yake..

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Hasna Mwilima akizungumzia sakata hilo amesema mahusiano baina ya mwekezaji na uongozi wa kijiji na Wilaya ni mzuri bali kinachojiri ni uwepo wa kikundi kidogo cha wakazi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakitumiwa na wanasiasa kwa maslahi binafsi.

Shamba la Kahawa la Burka lina ukubwa wa hekta mia tano na thelathini ambapo eneo hilo pia limekuwa likitumika kwaajili ya shughuli za utunzaji na uhifadhi wa mazingira ya asili kukiwa na takribani watumishi 2000 wanaofanya kazi shambani hapo.