Alhamisi , 12th Sep , 2019

Baadhi ya Madiwani wa Jiji la Dar es salaam wamesaini hoja ya kumtuhumu juu ya matumizi mabaya ya ofisi ya Umma Meya wa Jiji la Dar es salaam, Isaya Mwita, huku mwenyewe akihitajika kuwasilisha utetezi wake kesho Septemba 13, 2019.

Akizungumza na EATV/ EA Radio Digital Meya wa Temeke, Abdallah Chaulembo,  amesema 2 ya 3 ya Madiwani wa jiji hilo, wamekubaliana na hoja hiyo, na wameiwasilisha kwa Mkurugenzi wa jiji tangu, Septemba 5, 2019.

Chaulembo amesema kuwa "ni kweli tumesaini hoja ya kumtuhumu na kutokuwa na imani na yeye, ukisoma kanuni inajieleza sababu kwamba kama hamtakuwa na imani na yeye ni sawa kuandika hiyo hoja, na kanuni inasema 2 ya 3 Madiwani na sisi tumefika"

"Barua tumeandika toka tarehe 5, mwezi 9 na tulimpa Mkurugenzi na kama ilimfikia Mkurugenzi siku hiyo hiyo, maanake siku 5 zimeisha" ameongeza Chaulembo

Juhudi za kumtafuta Meya Isaya Mwita, ziligonga mwamba kutokana na simu yake kuita bila kupokelewa.

Mara baada ya kuwasilisha kwa utetezi wake, Mkurugenzi wa jiji anatarajia kuufikisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, ambaye yeye ataunda kamati ya kuchunguza tuhuma zake, ambapo kama ikithibitika anahatihati ya kupoteza nafasi yake.