Jumatatu , 2nd Mar , 2020

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Dkt Bashiru Ally, amemuomba aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe, aache kutapatapa na kwamba anahitaji kufanyiwa ushauri wa kisaikolojia ili aweze kuwa sawa.

Aliyekuwa mwanachama wa CCM Bernard Membe, kulia ni Katibu Mkuu wa CCM, Dkt Bashiru Ally.

Dkt Bashiru amesema kuwa anamtakia maisha marefu huko atakapoenda na kwamba anaamini kuwa licha ya Membe kufukuzwa uanachama ndani ya CCM,lakini anaamini ipo siku atarudi tena CCM kwa sababu milango ya kuwapokea wanachama wapya iko wazi.

"Namuona Membe, nadhani adhabu kubwa hii tumpe muda ni binadamu ana haki yake, asitapetape anahitaji ushauri nasaha, maana siyo tatizo dogo hili na mimi sitaki kulizungumza kwa ushabiki hata lingenipata mimi ningehitaji marafiki zangu wa karibu niwashirikishe" amesema Dkt Bashiru.

Februari 28, 2020, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Mwenyekiti wake na Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, kiliazimia kumfukuza uanachama, mwanachama wake wa muda mrefu Bernard Membe.