Jumamosi , 25th Jul , 2020

Mtia nia wa Urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo na kada wa zamani wa CCM Bernard Membe, ametoa rambirambi kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Rais wa Tanzania katika awamu ya tatu mwaka 1995 hadi 2005, Benjamin William Mkapa.

Bernard Membe

Membe ametoa salamu hizo za rambirambi akiwa mkoani Lindi, ambapo amesema kuwa chama chake kitaghairisha baadhi ya shughuli za chama kwaajili ya kushiriki safari ya mwisho ya Mkapa kwa kuanzia Dar es Salaam hadi kijijini kwao Lupaso.

''Mzee Mkapa tutamkumbuka kwa kuwa kiongozi ambaye alitumia wakati wake mwingi kuisaidia jamii ya Tanzania, ni miongoni mwa marais wazuri sana katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kifo chake kimetuletea majonzi watu wote'', amesema.

Aidha kada huyo wa ACT Wazalendo, amesema kuwa atamkumbuka Mzee Mkapa kwa elimu yake, ushauri, maagizo na mafundisho yake kuhusiana na masuala ya diplomasia ambayo amekuwa akiyasimamia enzi za uhai wake. Pia amezitaja nchi kama Burundi, Sudani , Kenya, Rwanda, Afrika Kusini na DR Congo kama nchi za mfano ambako Marehemu alitekeleza majukumu ya usuluhishi.

Hata hivyo Membe aliongeza kuwa dunia itamkumbuka mzee Mkapa kama mtu aliyejitolea maisha yake kuipigania Afrika yenye amani pasi na kuchoka.

Huku akigusia suala la Uchaguzi Mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, zaidi ameonesha wasiwasi wake na kusema kuwa ameondoka katika kipindi muhimu sana ambapo nchi inamhitaji zaidi.