Alhamisi , 8th Sep , 2016

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Ester Matiko (CHADEMA) ameitaka serikali kujenga gereza katika wilaya ya Rorya kutokana na msongamano wa wafungwa kuwa mkubwa katika gereza la Tarime wengi wakiwa wanatoka wilayani Rorya.

Ester Matiko (Kulia) akiwa kwenye kipindi cha HOTMIX, mwanzoni mwa mwaka huu, kushoto ni Mtangazaji wa kipindi, Belinda Semtandi

Akiuliza swali la nyongeza bungeni Dodoma Mbunge Matiko amesema magereza mengi nchini ni machakavu na katika gereza la Tarime linaingiza wafungwa wengi kutoka Rorya ambapo kwa hali ya kawaida linatakiwa kubeba wafungwa 209 lakini kwa sasa linabeba wafungwa hadi 600 jambo ambalo linasababisha msongamano mkubwa sana na kuitaka serikali itoe tamko ni lini itajenga gereza la wilaya ya Rorya.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni amesema serikali katika bajeti ya wizara yake mwaka huu imetenga bilioni 3 kwa ajili ya kukarabati na kumalizia baadhi ya magereza ambayo yalikuwa yameanzishwa na kuishia nusu.

Kuhusu gereza la Rorya Masauni amesema serikali itajenga magereza mapya kulingana na upatikanaji wa raslimali fedha .

Aidha katika eneo hilo hilo la magereza Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema serikali imetenga zaidi ya biloioni mbili kwa ajili ya kujenga magereza ya kurekebisha tabia za watoto pamoja na kujenga nyumba za wazee.