Alhamisi , 3rd Mar , 2016

MKOA wa Mbeya umetajwa kuwa moja kati ya mikoa nchini iliyo na tatizo kubwa la udumavu wa akili utokanao na lishe duni licha ya uwepo wa fursa kubwa ya upatikanaji wa aina mbalimbali ya mazao ya chakula.

Mratibu wa huduma za Uzazi na Mtoto mkoa wa Mbeya,Bibi Prisca Butuyuyu

Mratibu wa huduma za uzazi na Mtoto mkoa wa Mbeya, Bibi Prisca Butuyuyu amesema tatizo la udumavu wa akili ni kubwa zaidi mkoani hapa kwakuwa takwimu za mwaka 2013 zinaonesha kuwa mkoa una asilimia kubwa zaidi ya kiwango cha kitaifa cha tatizo hilo.

Bi. Butuyuyu amesema hayo alipozungumza na Kituo hiki akisema takwimu hizo zinaonesha wakati asilimia 42 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana udumavu nchini, mkoa wa Mbeya una asilimia 50 ya watoto walio na tatizo hilo.

Mratibu huyo amesema chanzo cha tatizo hilo ni jamii kutozingatia ushauri inayopewa katika vituo vya huduma za afya hususani ule unaotolewa na wataalamu kwa mama wajawazito na mara wanapojifungua.

Amesema jamii imekuwa ikiendelea kuishi kwa mazoea na kudharau ushauri wa lishe unaotolewa na wataalam ikiamini kuwa maisha yaliyozoeleka ndiyo mfumo sahihi pasipo kujua kuwa mambo yanabadilika kadiri siku zinavyokwenda.