
Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Mabadiliko hayo yametangazwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ambapo ameteua jopo la wahandisi saba kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema, ujenzi wa jengo jipya la Uwanja huo (Terminal Three) unaendelea hii leo mara baada ya mabadiliko hayo na kwamba hakuna tena mgomo kwani mkandarasi aliyetishia kusimamisha ujenzi atalipwa fedha zake mapema kama alivyoahidiwa jana na Rais Magufuli katika ziara yake.
Mafundi wa BAM wakiendelea na kazi
Awali mkandarasi anayejenga uwanja huo ambaye ni kampuni ya BAM International alitangaza kususia kuendelea na ujenzi huo kutokana na kutolipwa kiasi cha shiilingi bilioni 23 ambacho serikali imeahidi kukilipa haraka, hata hivyo Prof. Mbarawa amekiri kuwepo kwa mapungufu makubwa katika usimamizi wa mradi huo na kulitaka jopo jipya la wahandisi kusimamia mradi huo kikamilifu.
Ziara iliyofanya jana na Rais Magufuli katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam
Wakati huo huo Prof. Makame Mbarawa amemwondoa Mhandisi aliyekuwa akisimamia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mbeya baada ya kubaini kuwa mkandarasi aliyekuwa akijenga uwanja huo wa ndege wa Mbeya tayari alishalipwa fedha kiasi cha shilingi bilioni 3 licha ya kuwa amesimamisha ujenzi wa uwanja huo kwa madai ya kutolipwa fedha.