Meneja Mipango na Biashara wa Soko la Hisa la Dar es Salaam DSE, Bw. Patrick Mususa.
Meneja Mipango na Biashara wa soko hilo Bw. Patrick Mususa amesema hayo leo wakati akitoa taarifa ya biashara katika kipindi cha juma moja lililopita na kwamba katika kipindi hicho idadi ya hisa zilizouzwa nazo zimeongezeka mara sita kutoka hisa milioni moja na laki nne hadi hisa milioni tisa na laki moja.
Mususa amesema idadi ya mtaji wa soko imeshuka kutoka shilingi trilioni 22.2 hadi shilingi trilioni 21.8 huku mtaji wa makampuni ya ndani ukiwa umepanda kutoka shilingi trilioni 9.7 hadi shilingi trilioni tisa nukta nane.
Kampuni mbili zinazoongoza katika ongezeko la bei ya hisa ni Tanzania Oxygen Ltd kwa ongezeko la bei la asilimia 1.32 ikifuatiwa na Nation Media Group (NMG) kwa ongezeko la bei la asimilia 1.01.
Kuhusu viashiria ambavyo kwa lugha ya kitaalamu vinajulikana kama Indeces, Kiashiria cha sekta ya viwanda kimeshuka pointi 55.44 kikiwa kimechangiwa na punguzo la bei ya hisa kwenye kaunta ya TBL kwa asilimia 1.19 na TCCL kwa asilimia 2.63.
Kiashiria cha sekta ya huduma za kibenki na za kifedha kimeshuka kwa pointi 28.65 kikiwa kimechangiwa na punguzo la bei ya hisa kwenye kaunta ya DCB kwa asilimia 2.50 na NMB kwa asilimia 2.08.
Kiashiria cha sekta ya huduma za kibiashara kimeshuka pointi 50 kikiwa kimechangiwa na punguzo la bei ya hisa za SWISSPORT kwa hisa 1.60.
Aidha, soko la hisa linaendelea kutoa huduma kwa wananchi wote ambao wangependa kuja kuwekeza katika soko la hisa kupitia huduma ya kununua na kuuza hisa kupitia simu za kiganjani. Huduma hii inapatikana kwa simu ya mkononi ya mtandao wowote.