Timu ya EATV na EA Radio, kwa kushirikiana na aripads_tz, Hedhi Salama Marathon pamoja na TASACI, ilifanya ziara maalum katika Wilaya ya Chalinze kwa lengo la kuendeleza juhudi za kuhakikisha watoto wa kike wanapata hedhi salama.
Katika ziara hiyo, timu ilipokelewa kwa mapokezi makubwa, ya heshima na ya moyo wa dhati, hali iliyoonesha ushirikiano mzuri kati ya wadau wa maendeleo na uongozi wa Wilaya ya Chalinze. Mapokezi hayo yaliakisi dhamira ya pamoja ya kuunga mkono ustawi wa watoto wetu, hususan wanafunzi wa shule za msingi.
Shukrani za pekee na za dhati zinaelekezwa kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, kwa ushirikiano wake mkubwa na mchango wake katika kuhakikisha zoezi la ugawaji wa taulo za kike linafanikiwa. Ushirikiano huo umeiwezesha EATV na EA Radio kutimiza jukumu walilokabidhiwa na Watanzania la kuwasaidia watoto wa kike kupata mahitaji muhimu ya hedhi salama.
Ziara hii ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za pamoja za kuelimisha jamii, kuvunja ukimya kuhusu hedhi salama na kuhakikisha hakuna mtoto wa kike anayekosa fursa ya elimu kwa sababu ya changamoto za hedhi.




