Ijumaa , 30th Mei , 2014

Jeshi la polisi limekamata shehena ya mataruma ya reli yapatayo 331 yaliyoibiwa katika reli ya Tanga - Moshi Wilayani Korogwe mkaoni Tanga

Mataruma ya reli yaliyokamatwa

Zaidi ya Kilomita 5 za njia ya Reli ya kutoka Tanga kwenda moshi mkoani Kilimanjaro zimeibwa pamoja na mataruma zaidi ya 2700 hatua ambayo imeisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kurejesha mawasiliano yake kama kawaida.

Hatua inafuatia jeshi la polisi kukamata shehena ya mataruma ya reli yapatayo 331 yaliyokuwa yameibwa katika eneo la kijiji cha Goha Maguzoni kilichopo katikati ya kituo cha reli cha mkomazi na Mkumbara vilivyopo wilayani Korogwe kisha kuwatia mabroni watu watatu waliokiri kujihusisha na biashara ya vyuma chakavu.

Hata hivyo ongezeko la wizi huo wa nyara za serikali inadaiwa kuwa umetokana na waliokuwa wafanyakazi wa shirika la reli nchini TRL kuachishwa kazi na kusababisha nyumba walizokuwa wakiishi maarufu kama magenge kuvunjwa na watu wasiojulikana kwa sababu zipo porini na kusababisha kukosa ulinzi hatua ambayo maafisa wa shirika hilo wamependekeza ushikiano baina ya wana vijiji waliopo jirani na reli inapopita uimarishwe ili kupunguza kasi ya wizi wa nyara hizo.

Kufuatia hatua hiyo kaimu kamanda wa polisi mkoani Tanga Bwana Juma Ndaki amesema watatu wametiwa mbaroni na jeshi la polisi baada ya kukutwa wakiwa na mataruma ya reli 331 waliyokuwa wakisafirisha kama vyuma chakavu katika gari aina ya fusso kupeleka na jijini Dar es salaam baada ya jeshi la polisi kwa kushirikiana na wasamaria wema kubaini kuwa gari hilo lililokuwa limebeba pumba za mpunga lilikuwa na mataruma ya reli.