Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof Mussa Asad
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof Mussa Asad amesema changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa zinaweza kupata ufumbuzi na kukidhi matarajio ya watanzania kama viongozi na watendaji hasa walioko kwenye nafasi za maamuzi watakuwa tayari kutenda haki na kuweka mbele maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla .
Akizungumza baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa mwaka wa wakaguzi na wahasibu (NBAA) unaofanyika Arusha Prof Asad pamoja na kuwataka watanzania kuendelea kuwa na imani ya ofisi yake amesema pia tatizo la maamuzi ya kusukumwa na masuala ya kisiasa na maamuzi ya kusukumwa na maslahi binafsi ni kubwa na ni miongoni mwa vyanzo vya changamoto zinazojitokeza kwa sasa.
Akifungua mkutano huo Naibu Waziri wa Fedha Adamu Malima amewataka wakaguzi na wahasibu kufanya kazi kwa weledi na kulinda heshma ya taaluma zao na kutambua kuwa wana nafasi kubwa ya kusaidia kupatikana ama kutopatikana kwa ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa.
Naye mwenyekiti wa bodi ya wakaguzi na wahasibu (NBAA) prof Isaya Jairo amesema wanaendelea kuwajengea wahasibu uwezo wa kutekeleza majukumu yao na kuimarisha ushirikiano na wadau wengine na kwamba licha ya changamoto zilizopo kazi nzuri inayofanywa na ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ni kielelezo cha ufanisi mzuri wa wakaguzi na wahasibu