Jumatatu , 11th Jun , 2018

Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un wamewasili Singapore kwa ajili ya mkutano wao unaoelezwa kuwa wa kihistoria unaotaraji kufanyika kesho Jumanne.

Trump aliwasili saa chache tu baada ya Kim kuwasili katika kisiwa cha Sentosa, Marekani ina matumaini kuwa kukutana kwao utakuwa mwanzo wa mchakato ambao hatimaye itashuhudiwa Kim akiachana na mpango wake wa silaha za nyuklia.

Vyombo vya habari vya serikali Korea Kaskazini navyo vimesema mazungumzo hayo yanatoa fursa ya kuwepo kwa uhusiano mpya kati ya taifa hilo na Marekani.

Uhusiano wa viongozi hao wawili umepitia kwenye misukosuko kwa kipindi cha miezi 18 iliyopita, wakirushiana matusi na kutishiana vita kabla ya uhusiano wao kuchukua mkondo mwingine na kuamua wawili hao kukutana.