Jumamosi , 17th Feb , 2018

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri mtu mmoja kupigwa risasi na polisi wakati wakiwatawanya wafuasi wa CHADEMA walioandama jana Februari 16, 2018.

Kamanda Mambosasa amesema kuwa tukio hilo la mwanafunzi  (aliyejulikana kwa jina la Aqulina Akwilini Baftaha),   kupigwa risasi na Polisi  lilitokea wakati askari walipokuwa wakijaribu kutuliza fujo ambapo  walipiga risasi za moto na zikaweza kuwafikia wananchi takribani watatu ambapo mmoja kati yao amepoteza maisha.

Akizungumza na waandishi wa habari , leo Februari 17, Mambosasa amesema "Walizuia mwendo kasi, wakaanza kupiga mawe kwa hiyo kati ya risasi za hewani zilizopigwa kuwatawanya kuna iliyompata (mtu)".

Wafuasi hao wa CHADEMA wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliandamana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.

Maandamano hayo yalianzia viwanja vya Buibui Mwananyamala ulikokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni wa Chadema na yalipofika eneo la Mkwajuni wafuasi hao walitawanywa na polisi, huku mtu mmoja aliyekuwa kwenye basi la daladala akidaiwa kupigwa risasi na kufariki dunia.

Taarifa zinadai kuwa mwanafunzi huyo aliepoteza maisha kwa kupigwa risasi alikuwa safarini kulekea Bagamoyo kupeleka fomu za kuomba nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo (Field).

Akwilini anadaiwa kuwa alikuwa mwanafunzi  wa Chuo cha usafirishaji Tanzania (NIT) mwaka wa kwanza  jina na picha zake zilianza kusambaa jana jioni baada ya kutokea kwa tukio hilo.