
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja akizungumza na wadau
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo alipokuwa akifunga mdahalo wa masuala ya biashara ya hewa ya Kaboni jijini Dar es Salaam.
"Mpaka sasa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake zimepokea makapuni zaidi ya 20 kutoka nchi za Kenya, Urusi, Singapore, Marekani, Kanada, Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Uswisi, Estonia, na Italia kuja kuwekeza katika biashara ya hewa ya Kaboni," amesema Naibu Waziri Masanja.
Amesema nchi hizo zimeshaingia makubaliano ya awali na Tanzania na baadhi ya mazungumzo yanaendelea kwenye taasisi husika chini ya usimamizi wa Kituo cha Uratibu wa Masuala ya Hewa ya Kaboni kilichopo mkoani Morogoro (NCMC).
Masanja ametaja maeneo yanayotarajiwa kuingia katika uwekezaji huo kuwa ni misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu,Misitu ya Vijiji, Miradi ya Upandaji Miti, Hifadhi za Wanyamapori za Jamii, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Taifa.
Biashara ya Hewa ya Kaboni ni sehemu ya utekelezaji wa kifungu (article 6.2) cha Makubaliano ya Mkataba wa Paris unaolenga kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.