Ijumaa , 5th Oct , 2018

Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutokana na kasoro za kikanuni katika hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Uamuzi huo wa mahakama ulioandaliwa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, Dalum Mbarouk (mwenyekiti wa jopo), Shaban Lila na Jacobs Mwambegele, umesomwa leo Ijumaa Oktoba 5, 2018 na Naibu Msajili, Eddy Fussi ambapo kasoro hizo ni hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufaa kutobainisha kiini cha uamuzi au amri ya Mahakama Kuu waliokuwa wakiukatia rufaa

Naibu Msajili Fussi amesema kwa kuwa taarifa ya kusudio la kukata rufaa kwenye kesi za jinai ndio msingi wa rufaa, kutupwa kwake kunaifanya hata rufaa yenyewe kukosa uhalali au msingi wa kusimama.

Katika rufaa hiyo, viongozi hao wa Chadema walikuwa wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na Jaji Rehena Sameji, kutupilia mbali maombi yao ya mapitio ya mwenendo wa kesi yao ya msingi ya jinai inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupitia kwa jopo la mawakili wa Serikali, likiongozwa na wakili wa Serikali Mkuu Paul Kadushi aliweka pingamizi, pamoja na mambo mengine akisema kuwa maombi hayo ni batili kwakuwa yanakiuka Sheria ya Mahakama za Hakimu Mkazi.

Mbali na Mbowe, wengine Katika rufaa hiyo na ambao wote wanakabiliwa na kesi ya msingi ya jinai Kisutu ni pamoja na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji. Wengine ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar), mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 ambayo ni kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali yanayowakabili wote, huku Mbowe, Msigwa Mdee na Heche kila mmoja peke yake akikabiliwa na mashataka zaidi.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16 katika barabara ya Kawawa, Mkwajuni, Kinondoni, siku wakihitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni na kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.