Jumatano , 4th Feb , 2015

Tanzania leo imeadhimisha siku ya sheria ambayo huashiria kuanza kwa mwaka mpya wa idara ya mahakakama, ambapo Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye ameitaka serikali kuoboresha majengo na mazingira ya kazi katika idara ya mahakama.

Wilayani Hanang' waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye aliyeshiriki maadhimisho hayo, ameitaka serikali kuboresha majengo ya mahakama za mwanzo katika kata ambazo hazina mahakama hizo.

Sumaye pia ameshauri serikali kupanua majengo ya magereza ili kuondoa msongamano na kutoa nafasi kwa mahakimu kufanya kazi kwa ufanisi na kuondoa hisia za rushwa.

Nao viongozi wa madhehenu ya dini mjini katesh wamehimiza serikali kusimamia utekelezaji wa haki huku wakiwalaumu baadhi ya watendaji wa serikali kujikita kwenye vitendo vya rushwa.

Sumaye ametoa kauli hiyo mjini katesh kwenye sherehe za siku ya sheria baada ya kuombwa toka nyumbani kwake katika kijiji cha Endasiwold kata ya Endasak kuhudhuria sherehe hizo kama mdau wa serikali na waziri mkuu mstaafu,amesema ingawa kumekuwa na maboresho ya kumaliza mashauri haraka na kutoa hukumu kwa wakati lakini anashangazwa na baadhi ya walalamikaji wa mashauri kulalamikia utendaji huo wakidai mahakami wanafanya hivyo kutokana na visa.

Awali katika hotuba ya hakimu mkazi mfawidhi wilayani hanang  Saidi Rashidi Ding’ohi mbele ya wadau mbalimbali na watumishi wa serikali amesema ingawa jengo la mahakama ya wilaya ya Hanang kuwa bovu na chakavu na baadhi ya kata hazina mahakama za mwazo lakini mahakakama hizo zimefanikiwa kufikia malengo ya kumaliza mashauri 250 kwa mwaka kama wajibu wa serikali katika kuwezesha fursa ya upatikanaji wa haki wilaya Hanang.

Hata hivyo licha ya viongozi wa madhehenu ya dini mjini Katesh wakiihimiza serikali kusimamia utekelezaji wa haki huku wakiwalaumu baadhi ya watendaji wa serikali kujikita kwenye vitendo vya rushwa, mkuu wa wilaya ya Hanang ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi Christina Mndeme amewataka watendaji wakiwemo mahakimu na polisi kutenda haki kwani hakuna aliye juu ya sheria.

Mkoani Mara wananchi wa mkoa huo waoshiriki maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika kimkoa mjini Musoma, wamekemea vitendo  vya  rushwa  na ubambikizwaji wa  kesi  unaodaiwa  kufanywa  na  baadhi  ya  askari  wa  jeshi la  polisi.
Wananchi hao wamedai kuwa hiyo ni  moja  ya  sababu  ambayo imechangia mrundikano  wa  wafungwa  na  mahabusu magerezaji,  hatua  ambayo  imefanya  serikali  kutumia  gharama  kubwa  kuwatunza wafungwa  na  watuhumiwa  ndani  ya  magereza hayo.