Jumatatu , 5th Dec , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemaliza mgogoro wa ardhi  uliodumu kwa miaka 17 kati ya vijiji viwili vya Ortukai na Esilalei na Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT) wilayani Monduli, mkoani Arusha

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Mto wa Mbu wilayani Monduli akiwa katika ziara ya mkoa wa Arusha.

Amemaliza mgogor huo baada ya kukabidhi hati ya  shamba la Manyara Ranch  kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulaya.

Hati hiyo imetolewa jana jioni Waziri Mkuu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Mto wa Mbu kwenye viwanja vya Barafu baada ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi wa vijiji  hivyo vilivyopo kwenye  Kata ya Elesilalei Wilayani Monduli Mkoani Arusha.

Hatua hiyo imekuja baada ya kilio cha muda mrefu cha wananchi hao kudai kuwa Rais wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliagiza shamba hilo ligawiwe kwa wananchi hao lakini jambo hilo halikufanyika na badala yake watu wachache walijimilikisha shamba hilo kinyemela chini ya wenyekiti wa bodi ya TLCT.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameshika ngao na Mkuki alivyopewa na Mzee wa Mila wa kabila la Wamasai, Laibon Meshuko Ole Mapii (kulia) kabla ya kuwahutubia wananchi kwenye shule ya msingi ya Laibon iliyojengwa na Laibon Ole mapii na kukabidhiwa kwa serikali

 

Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kurudisha umiliki wa shamba hilo kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili baada ya Baraza la Madiwani na Uongoziwa Wilaya hiyo ya Monduli kuridhia kwa pamoja umiliki huo kurudi kwa wananchi kama ilivyoamriwa hapo awali.

"Shamba hili lenye ukubwa wa ekari 44,930 sasa si mali tena ya Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT) iliyokuwa inafadhiliwa na Shirika la African Wildlife Foundation (AWF) sasa ni mali ya wananchi na halmashauri ya wilaya ya Monduli ndio itapanga matumizi bora ya ardhi ya shamba hili mliloteseka nalo kwa muda mrefu ," alisema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utlii, Profes Jumanne Maghembe baada ya kuwahutubia wananchi kwenye shule ya msingi ya Laibon wilayani Monduli Desemba 4, 2016. Katikati ni Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amempa siku mbili Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mazingira wa wilaya ya Monduli , Adil Mwanga kumuondoa muwekezaji, Lekisongo Meijo katika shamba lenye ukubwa wa ekari 2,800 lililoko katika kijiji cha Lemoti tarafa ya Kisongo ambalo alimilikishwa bila ya kufuata taratibu na kulirudisha kwa wananchi.

Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Gambo kufanya uchunguzi wa umiliki wa mashamba mengine makubwa ambayo yana migogoro na  hayajaendelezwa mkoani humo likiwemo la Makuyuni Stein Seed Valley na  kuipatia  ufumbuzi migogoro hiyo.