Alhamisi , 7th Mar , 2019

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,  imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwafutia dhamana Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, ambapo wameruhusiwa kuwa nje kwa dhamana.

Mwenyekiti CHADEMA, Freeman Mbowe

Akitoa uamuzi huo mahakamani leo Alhamisi Machi 7, Jaji Sam Rumanyika, amesema Mahakama imeikubali rufani hiyo kama ilivyo  hivyo warufani wanatakiwa wawe nje  na kwamba uamuzi wa kuwafutia dhamana ulifanyika mapema mno (pre mature).

“Aidha, sharti la kuripoti polisi kila alhamisi limefutwa badala yake watariporti mahakamani mara moja kwa mwezi si polisi tena kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Kisutu mara ya kwanza,” amesema.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwafutiwa Mbowe na Matiko dhamana kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana hiyo ambapo walikata rufaa Mahakama Kuu Desemba mwaka jana na uamuzi kutolewa leo.

Walifutiwa dhamana hiyo na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri Novemba 23, 2018 lakini siku hiyohiyo kupitia kwa wakili wao Peter Kibatala walikata rufaa Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura sana wakipinga uamuzi huo.