Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini -TUCTA limelaani maamuzi ya mahakama kuu kitengo cha kazi cha kuwataka wafanyakazi zaidi ya1500 wa mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia-TAZARA- kurudi kazini na kuendelea na kazi bila kuiamuru menejimenti ya mamlaka hiyo kulipa mishahara ya miezi 6 wanayodai.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hukumu iliyotolewa na mahakama mkuu kitengo cha kazi, katibu wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi-TUCTA- Bwana Hezron Kaaya amesema wafanyakazi wa TAZARA hawajagoma kwenda kazini ila hawana nauli kutokana na kukosa mishahara kwa miezi sita.
Pia ametoa siku tano kwa menejimenti ya TAZARA kulipa mishahara yote kabla hawajachukua hatua stahiki ya kushirikisha wafanyakazi wote kupitia vyama vyao kuchukua hatua.
Katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa reli- TRAWU- Bwana Erasto Kihwele amesema wafanyakazi wa TAZARA wamehuzunishwa na hukumu ya mahakama kuu kitengo cha kazi ya kuwataka kurudi kazini wakati hawana mishahara kwa miezi sita, ambapo amesema kufuatia maamuzi hayo wamepanga kukutana na wafanyakazi ili kuamua hatua za kuchukua dhidi ya hukumu hiyo.
Zaidi ya miaka 10 ya wafanyakazi hao imekuwa ikikumbwa na migomo na migogoro kati ya wafanyakazi na menejimenti kuhusu tatizo la kutolipwa mishahara pamoja na matatizo ya uendeshaji wa kampuni hiyo na kusababisha idadi kubwa ya wafanyakazi na baadhi ya viongozi wa kampuni hiyo waondolewe.