Jumapili , 5th Jun , 2016

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaalika wawekezaji kutoka Jimbo la Jiangsu la nchini China kuungana na Tanzania katika utekezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda na ujenzi wa miundombinu hususani reli.

Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na wageni wake kutoka Nchini China.

Rais Magufuli ametoa mwaliko jana Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa Jimbo la Jiangsu Mheshimiwa Luo Zhijun ambaye yupo hapa nchini akiwa na viongozi wengine wa serikali wa jimbo hilo kwa ziara ya kikazi.

Dkt. John Pombe Magufuli amemueleza Mheshimiwa Luo Zhijun kuwa serikali yake ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha asilimia 40 ya watanzania wanapata ajira kupitia viwanda ifikapo mwaka 2020, hivyo ili jitihada hizo zifanikiwe inawakaribisha wafanyabiashara wa Jiangsu kuanzisha viwanda vitakavyosindika na kuzalisha bidhaa za mazao ya kilimo na ufugaji yakiwemo pamba, kahawa, korosho, samaki na nyama kwa kuwa malighafi zipo na pia fursa za kupanua uzalishaji wa malighafi hizo zipo.

Amemhakikishia Kiongozi huyo wa Jimbo la Jiangsu ambalo lina viwanda vingi nchini China kuwa licha ya uwekezaji wa viwanda kuinufaisha Tanzania kwa wananchi wake kupata ajira na serikali kukusanya mapato, wawekezaji wa China watanufaika na fursa ya soko kubwa la ndani ya Tanzania na nchi saba zinazoizunguka Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zenye watu zaidi ya milioni 650.

"Mheshimiwa Luo Zhijun naomba uwaeleze wafanyabiashara wa Jimbo lako la Jiangsu kwamba ninawakaribisha kwa mikono miwili, waje hata kesho waseme wanataka kuanzisha kiwanda gani na sisi tutawapa ushirikiano.

"Tunayo maeneo ya kutosha ya kuanzisha viwanda, kwa Pwani na Dar es salaam tuna eneo la Bagamoyo tunaloweza kuweka viwanda zaidi ya 1,000 halikadharika Kigamboni na maeneo mengine mengi katika mikoa mbalimbali nchini nzima" Amesema Rais Magufuli.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli pia amemueleza Mheshimiwa Luo Zhijun kuwa serikali yake inayakaribisha makampuni ya Jiangsu kuungana na Tanzania katika ujenzi wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kati ambao tayari Tanzania imetenga shilingi Trilioni 1 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) katika bajeti ijayo, ujenzi wa kilometa 1,200 za barabara ya njia sita kutoka Dar es salaam hadi Chalinze na miradi mingine.

Kwa upande wake Mheshimiwa Luo Zhijun amemshukuru Rais Magufuli kwa utayari wake wa kuwapokea wawekezaji kutoka Jimbo la Jiangsu na amemuahidi kuwa pamoja na kwamba Jimbo hilo tayari limewekeza hapa nchini kiasi cha dola za Marekani Bilioni 1 (Sawa na Shilingi Trilion 2.2) atahakikisha anawashawishi wawekezaji wengi zaidi wa viwanda katika jimbo lake, kuja Tanzania haraka iwezekanavyo ili kufanikisha mpango wa kujenga viwanda na kuzalisha ajira.

Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing aliyeambatana na Mhe. Luo Zhijun amemueleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kuwekeza Dola Bilioni 1 kati ya Dola Bilioni 6.62 zilizowekezwa na China hapa nchini kwa mwaka 2014/2015 wawekezaji wa jimbo la Jiangsu wanakusudia kuwekeza Dola za Marekani Bilioni 5 (Sawa na Shilingi Trilion 11) nchini Tanzania katika miaka mitano ijayo.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda ambaye jana tarehe 03 Juni, 2016 ametiliana saini makubaliano ya ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Mkoa wa Dar es salaam na Jimbo la Jiangsu ambapo jimbo hilo limeahidi kuwekeza katika miradi mbalimbali ya viwanda vya mazao ya kilimo, ujenzi na huduma za kijamii.