MHE. PAVEL REZAK -BALOZI WA JAMHURI YA CZECH HAPA NCHINI.
Balozi wa kwanza kukabidhi hati zake za utambulisho kwa Rais Magufuli ni Mheshimiwa Carlos Alfonso Iglesias Puente, Balozi wa Brazil hapa nchini ambaye ameahidi kuwa Brazil ipo tayari kuimarisha zaidi uhusiano wake na Tanzania, na ametaja maeneo ya uzalishaji wa zao la Pamba na Miwa kuwa ni miongoni mwa yatakayozingatiwa.
Kwa upande wake Rais Magufuli amemhakikishia Balozi Carlos Alfonso Iglesias Puente kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na Brazil, na pia ametaka uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Brazil uimarishwe zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inazo rasilimali na fursa nyingi zinazoweza kutumika kwa faida ya pande zote mbili.
Balozi wa pili aliyekabidhi hati zake za utambulisho ni Mheshimiwa Pavel Rezac, Balozi wa Jamhuri ya Czech hapa nchini, ambapo katika mazungumzo yao Rais Magufuli ameialika Jamhuri ya Czech kuungana na Tanzania katika juhudi zake za kuendeleza kilimo na kuzalisha umeme kwa kutumia gesi, ambayo mpaka sasa Tanzania imefanikiwa kugundua uwepo wa futi za ujazo zaidi ya Trilioni 57.
Rais Magufuli pia amemuomba Balozi Pavel Rezac kumpelekea salamu Rais wa Jamhuri ya Czech Mheshimiwa Milos Zeman, na kumhakikishia kuwa Serikali yake ya awamu ya Tano ipo tayari kuimarisha zaidi ushirikiano na Jamhuri ya Czech, kukuza biashara na uwekezaji na kujenga mahusiano imara zaidi.
Balozi wa tatu aliyekabidhi hati zake za utambulisho ni Mheshimiwa Mariano Deng Ngor, Balozi wa Sudani Kusini hapa nchini ambaye amewasilisha salamu za Rais wa Sudan Kusini Mheshimiwa Salva Kiir, na kueleza kuwa nchi hiyo itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Tanzania, huku ikitambua na kuheshimu mchango mkubwa unaotolewa na Tanzania katika kutatua mgogoro wa kisiasa nchini mwao.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Tanzania itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na Sudan Kusini, na pia ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa taifa hilo changa kufanya biashara moja kwa moja na Tanzania na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambazo sasa idadi yake ya watu imefikia milioni 165.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli ameagana na Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim ambaye hivi karibuni alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait.
Mheshimiwa Balozi Mahadhi Juma Maalim anakwenda kuanzisha Ofisi za Ubalozi nchini Kuwait, ikiwa ni moja ya juhudi za Tanzania kuimarisha na kuongeza ushirikiano na uhusiano wake na nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.







