Jumatatu , 25th Mei , 2015

Watalamu na watafiti wa mazao ya kilimo wameonyesha matumaini ya kudhibiti magonjwa yanayoshambulia mazao ya Migomba na Mhogo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, baada ya kubuniwa kwa teknolojia ya vipando vya mimea hiyo.

Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo kutoka Wizara ya Kilimo na Ushirika Dakta Fidelis Mnyaka

Magonjwa yanayotajwa kushambulia mazao hayo kwa wingi ni pamoja na Mnyauko kwa upande wa migomba, hususani katika eneo la Kagera Tanzania, na ugonjwa wa Batobato na Michirizi ya Kahawia unaoshambulia zao la Mhogo.

Katika kutekeleza azma hiyo wataalamu na watafiti katika sekta ya kilimo wamekuta Jijini Arusha, ili kutathimini njia za kusambaza teknolojia hizo kwa wakulima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Africa Harvest lenye Makao yake makuu nchini Kenya Dakta Florence Wambughu, amesema kupitia ufadhili kutoka kwa Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya Kilimo (IFAD),mpango huo unalenga kuvishirikisha vituo vya utafiti wa mazao na kuwasambazia wakulima teknolojia hiyo mpya, ili kuongeza usalama wa chakula..

Awali Akizungumza katika Mkutano huo Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo kutoka Wizara ya Kilimo na Ushirika Dakta Fidelis Mnyaka, ameeleza kwamba Serikali ya Tanzania, inaangazia kuona kilimo kinakua kwa kasi kuliko ilivyo sasa kupitia mpango wa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi yaani PPP ambapo vituo vya utafiti vitakuwa na fursa pana ya kusambaza teknolojia mpya kwa wakulima.

Kwa upande wa Tanzania teknolojia hizo zinatarajiwa kusambazwa katika Wilaya za Misenyi na Muleba Mkoani Kagera, na huko Kenya ni katika kaunti ya Nyamira mbapo wakulima zaidi ya elfu kumi wanatarajiwa kufikiwa katika nchi za Afrika Mashariki.