Kaskazini mwa Nigeria imeathirika zaidi na mafuriko, kwa mujibu wa Manzo Ezekiel, ambaye anazungumza kwa niaba ya Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Dharura (NEMA).
Maeneo mengine ya nchi hata hivyo bado yako hatarini, aliongeza, huku kukiwa na mvua kubwa na viwango vya maji vinavyoongezeka vya mito yake miwili mikubwa - Niger na Benue.
Ingawa sehemu za Nigeria zinakabiliwa na mafuriko wakati wa msimu wa mvua, Ezekiel alisema mafuriko ya mwaka huu yameripotiwa katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa nadra.
Zaidi ya watu 600 walipoteza maisha katika mafuriko kote nchini humo mwaka 2022, ikiwa ni idadi mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Mamlaka zilihusisha mafuriko hayo na mvua za juu ya wastani na kufurika kwa bwawa la Lagdo nchini Cameroon.
Wiki iliyopita, Shirika la Huduma za Hydrological Nigeria (NIHSA) lilionya kuwa maji ya mafuriko kutoka nchi jirani za Niger na Mali "yanatarajiwa kuhamia hatua kwa hatua nchini Nigeria" huku likiyataka majimbo yaliyo kando ya mto Niger kuwa katika hali ya tahadhari.