Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Ametoa wito huo leo Jumanne, Agosti 20, 2024 wakati akifungua kongamano la siku tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST) kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa (AICC) jijini Arusha.
"Wakuu wa taasisi hakikisheni madereva wanapata stahiki zao kikamilifu kwa kuzingatia sheria, ni muhimu posho ya kujikimu nje ya vituo za safari zilipwe kulingana na siku za safari na stahiki za wahusika wenyewe na posho za sare zitolewe kwa wakati ili wawe smart," amesema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu amesema madereva hawana budi kuandaliwa mafunzo kazini na waajiri wao na kulipiwa gharama husika ili kuboresha umakini na utendaji kwa kuzingatia mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia.
Amesema waajiri waangalie utaratibu wa kazi za madereva wao na bila kuathiri utekelezaji wa majukumu, wawawekee ratiba zinazowawezesha kupata muda wa kupumzika.
Amewataka madereva wa serikali wawe mfano wa kuigwa kwa madereva wote kwa kuzingatia majukumu yao kwa umakini na kwa heshima; watunze vyombo vyao vya usafiri na washirikiane na timu za matengenezo ili kuhakikisha kuwa magari ya Serikali yanaendelea kuwa katika hali bora ya kuendeshwa.
Kuhusu usalama na utunzaji wa siri, Waziri Mkuu amewataka madereva wazingatie suala hilo kwa kutunza nyaraka za ofisi na kuhakikisha mazungumzo wanayoyasikia wakiwa katika majukumu yao hayafiki kwa wasiohusika.