Jumatatu , 30th Jun , 2014

Madereva wa pikipiki maarufu kama boda boda katika Jiji la Dar es Salaam wamelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi na kuwabaini watu wanaojiita polisi shirikishi ambao wamekuwa wakiwakamata mara kwa mara na kuwatoza faini hata kama hawana makosa.

Mkuu wa kikosi cha polisi wa usalama barabarani, kamanda Mohammed Mpinga.

Madereva hao wa boda boda wamesema kitendo cha wao kuzuiwa kufika kati kati ya Jiji kumesababisha baadhi ya watu kutumia nafasi hiyo kwa kuwakamata kwa madai wamekwenda kinyume na sheria za usalama barabarani na pale wanapolipa faini na kudai risiti wanatishiwa kupelekwa polisi.

Wakati huohuo, wakazi na madereva wanaotumia barabara ya Tandale Uzuri jijini Dar es Salaam, wameiomba serikali kuifanyia ukarabati barabara hiyo kutokana na kuwa na mashimo makubwa yanayosababisha kujaa maji wakati mvua inaponyesha.

Wamesema nyakati za usiku kumekuwa kukitokea ajali za mara kwa mara katika eneo hilo huku magari yakipita kwa shida jambo ambalo wamesema ni hatari na linahitaji kutatuliwa ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea.