Jumamosi , 30th Mei , 2015

Mbunge wa jimbo la Monduli kupitia Chama Cha Mapinduzi na Waziri Mkuu wa Zamani Mh. Edward Lowassa leo ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akitaja sababu zilizomfanya kugombea nafasi hiyo.

Akihutubia maelfu ya Wananchi waliojitokeza katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Mh. Lowassa amesema nchi kwa sasa inahitaji rais mwenye sifa kama alizokuwa nazo ikiwemo na kufanya maamuzi magumu pamoja na kupmbana na rushwa kwa vitendo.

Aidha Mh. Lowassa amesema amejitokeza kuwanianafasi akiwa na vipaumbele katika kuinua vijana katika sekta ya ajira, kusimamia Muungano, Kuinua sekta ya Elimu pamoja na kunyanyua uchumi wa nchi kupita rasilimali ilizonazo.

Ameongeza kuwa kuwa atakahikikisha anawekeza katika sera ya elimu ambapo ndio muhimili mkubwa katika maendeleo ya nchi hivyo ataweza kufanya hivyo atakapopewa ridhaa ya chama chake kuweza kugombea nafasi hiyo.

Lowassa amesema ameamua kugombea urais ili kupambana na umasikini ambapo amesema Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zinahitaji uongozi bora ili kuweza kuitoa nchi katika umasikini.

Mengine atakayo yapa kipaumbele ni pamoja na kutatua migogoro ya ardhi na wakulima na wafugaji lakini na kuyaenzi mapinduzi pamoja kudumisha uzalendo wa nchi kwa wananchi.

Katika sekta ya michezo, Lowassa amesema atahakikisha Tanzania inafanya vizuri katika ramani ya dunia ili isiendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu na kwamba ataweka mkazo zaidi katika mchezo wa riadha.

Aidha ameongeza kuwa atalishughulikia tatizo la foleni za jiji la Dar es salaam kwa miezi kumi na mbili endapo mpaka akiingia madarakani ikiwa bado tatizo hilo halijatatuliwa.

Katika hotuba take hiyo iliyorushwa moja kwa moja na vituo mbalimbali vya Radio na Televisheni ikiwemo vya East Africa TV na East Africa Radio Mh. Lowassa amesema yeye anachukia sana umasikini.

Mh.Lowassa amesema lengo lake ni kukuza uchumi wa Tanzania na kuondokana kuwa bakuli la ombaomba na kuwa nchi ya neema.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wengi wa Chama cha Mapinduzi akiwemo mwanasiasa Mkongwe nchini Kingunge Ngombare Mwiru ambaye alipopata machache ya kuongea alisema nchi sasa inahitaji Kiongozi kama Edward Lowassa.

Akimuelezea Lowassa, Kingunge amesema kuwa Lowassa ni mtu ambaye amelelewa ndani ya chama na kupata misingi yote ya maadili ya kitanzani na ya CCM, pia ni miongoni mwa viongozi ambao walipitia utaratibu wa chama wa kupitia jeshini akiwa pamoja na Kikwete, Kinana n.k

Mwisho mzee Kingunge amesema kwa niaba ya wazee ndani ya chama, anamuunga mkono Lowassa na kumshauri yeye pamoja na makada wengine kusameheana kwa lolote ambalo wamekoseana.
"Hata sisi zamani ilikuwa tukikanyagana tunayaacha na tunasonga mbele, safari ya matumaini ndiyo imeanza, mpaka kieleweke" Amesema Kingunge