Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa
Edward Lowassa ndiye mtu pekee ambaye ameweka rekodi ya kuwa mgombea urais pekee ambaye alitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Chama cha upinzani tena akiwa ni Waziri Mkuu Mstaafu aliyekuwa na ushawishi mkubwa na kudumu upinzani kwa muda wa siku 1312.
Marchi 1, 2019 Edward Lowassa alitangaza uamuzi wa kurejea CCM kwa kutoa kauli kuwa "nimerudi nyumbani", licha ya kwamba Julai 2015 wakati akitangaza kuhama, alitoa kauli akisema, "CCM si Baba yangu wala si Mama yangu".
Kwa kauli hizo mbili za, "CCM si Baba yangu wala si Mama yangu" na "nimerudi nyumbani", Lowassa anasomeka kama kiongozi ambaye amedhihirisha nguvu yake kubwa ndani ya CCM wakati anahama na upande wa upinzani tangu kuanza mfumo wa vyama vingi kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho.
Kiongozi ambaye alikuwa akishikilia mafanikio ya upatikanaji wa kura nyingi upande wa upinzani kabla ya Lowassa ni aliyekuwa Dkt Wilbard Slaa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambaye alipata jumla ya kura milioni 2.2 ambazo ni sawa na asilimia 27.
Upande wa Edward Lowassa yeye alipata jumla ya kura milioni 6 na kupata ushindi wa asilimia 39 na kumfanya kufikia rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na vyama vya upinzani nchini.
Kuna mitazamo mingi juu ya kurudi kwake CCM lakini yote yatabaki nadharia tu ambazo haiwezi kuzuiliwa japo mwisho wa siku kinachoweza kusemwa ni kwamba ametumia haki yake ya kikatiba kushiriki siasa ndani ya chama chochote kama ambavyo aliitoa wakati Mbunge wake wa Monduli, Julius Kalanga alipofanya maamuzi ya kuhama CHADEMA na kuhamia CCM.
