Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 21, 2020, wakati akizungumza mubashara kupitia channel ya Youtube ya chama hicho na kueleza kuwa licha ya kwamba ameamua kurudi nchini lakini bado yuko kwenye hatari zaidi kwa kuwa wale waliomshambulia na kumjeruhi bado hawajulikana hivyo anayo imani kwamba bado wapo.
"Baada ya miaka karibu mitatu ya matibabu, wakati wa mimi kurudi nyumbani umewadia, kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7, 2017, nitakanyaga ardhi na udongo wa Tanzania siku ya Jumatatu, Julai 27, 2020, Mjini Dar es Salaam, majira ya saa 7:20 mchana na nitaingia na Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia" amesema Tundu Lissu.
Akizungumzia suala la usalama wake Lissu amesema, "Wale waliokuja kuniua miaka mitatu iliyopita na waliowatuma, bado wanaitwa watu wasiojulikana, maana yake ni kwamba bado wapo, na hawajasema kama lengo lao la kuniua wameliacha bado kuna hatari ya maisha yangu, ninarudi nchini katika mazingira ambayo hatari dhidi yangu haijaondoka bado, lakini narudi tu ni nyumbani kwetu".








