Mbunge wa Arusha Mjini - Godbless Lema
Akisoma uamuzi mdogo wa Jaji Fatuma Masengi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angero Rumisha, alisema kuwa Mahakama imeifuta Rufaa hiyo, kutokana na wakata rufaa kuikata nje ya muda.
Rumisha amesema waomba rufaa walitakiwa kuonesha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku kumi tangu maamuzi ya maombi ya marejeo kutupwa na Mahakama Kuu, yaliokuwa mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Sekela Moshi Novemba 11.
“Hivyo,mwomba rufaa hii Lema kupitia mawakili wake alitakiwa kuonesha kusudio au kutoa notisi kuonesha mahakama sababu ya kukata rufaa na Novemba 21 walipaswa kukata rufaa lakini wao wamekata Novemba 22 nje ya muda wa kukata rufaa,” alisema.

Amesema kutokana na hivyo, Mahakama imekubaliana na upande wa pingamizi lililowekwa na upande wa serikali kupitia Wakili Paul Kadushi akishirikiana na Martenus Marandu kuwa rufaa hiyo haikufuata misingi ya kisheria kuikata sababu hakuna kusuidi la kukata rufaa na kuiomba mahakama hiyo itupilie mbali rufaa hiyo.
Rumisha alisema baada ya pingamizi hilo kutolewa na upande wa Lema kuomba Mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo kwani rufaa yao ipo ndani ya muda na imewasilishwa kwa hati ya dharura, Rumisha alisema Mahakama ilivyopitia hoja za pande zote mbili imeona rufaa hiyo imeletwa Mahakamani hapo nje ya muda unaotakiwa.
Aidha alisema mbali na nje ya muda pia wakata rufaa hawakuzingatia sheria inavyotaka kuwa ukikata rufaa lazima uanze na kutoa siku kumi za kusudio la kukata rufaa, jambo ambalo wanaifutilia mbali rufaa hiyo.

John Mallya - Wakili wa Lema
Nje ya Chumba cha Mahakama
Wakili wa Lema, John Mallya akizungumza na waandishi wa habari, amesema wamezungumza na mteja wao mara baada ya maamuzi ya Mahakama hiyo naye amewaomba kutojishughulisha na suala lolote la kukata rufaa, ingawa wao kama Mawakili wanaona bado kuna njia za kufanya hivyo Mahakama za juu.
Lema akiwa na mkewe Neema Lema
Mke wa Lema Neema Lema akiwa na watoto wake wawili amesema
“Nashukuru watu wote waliojitokez akuja katika kesi hii, licha ya usumbufu mwingi waliokutana nao ila hawakukata tama, ila kama familia na nilipoongea na mume wangu Lema tumeona kuwa katika kesi hii kuna mtu anataka Mahakama ifuate maagizo yake, hivyo nasi tumeona aachwe huyo mtu yafuatwe maagizo yake na afanye atakalo, mume wake atakaa Kisongo,”alisema Neema Lema.
Alisema wamekubaliana kutofungua kesi yoyote mpaka hapo huyo mtu atakapoona inafaa kuacha au la, ila wanachofahamu Tanzania hakuna mwenye hati miliki, iwe kiongozi yoyote mwenye cheo chochote watapita tu tawala zao na maisha yataendelea.








