Ikulu
ASKOFU wa Kanisa la Tanzania Field Evangilism (TFE) la Mjini Shinyanga, Edsoni Mombeki amewatahadharisha wananchi kuwa makini na viongozi wanaotangaza nia mapema ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kwa kuhofia kupata viongozi wasio na sifa ambao baadaye wanaweza kuiyumbisha nchi.
Ametoa tahadhari hiyo kanisani kwake, wakati akifunga maombi ya siku tatu ya kuliombea taifa amani hasa wakati huu linapojiandaa na kuipigia kura katiba mpya inayopendekezwa na kuelekea uchaguzi mkuu ili kuwapata viongozi wazalendo na waandilifu watakaoweza kuleta ukombozi wa kimaendeleo kwa wananchi.
Amesema, wananchi wanapaswa kuwa makini na viongozi wanaotangaza nia hiyo ya kusaka urais mapema kabla ya mchakato rasmi kuanza na kuwataka kuwachunguza kwa macho matatu na kutahadharisha kuwa mtu anaye kimbilia kwenda ikulu bila ridhaa ya wananchi siyo mzuri na hawezi kuiongoza nchi.
Hata hivyo askofu huyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha na kuipigia kura Katiba mpya inayopendekezwa na kuwa kitambulisho hicho pia ndicho kitakacho tumika kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambayo ndiyo itakuwa njia pekee ya kuchagua viongozi walio na sifa, wazalendo, na wenye kuiongoza nchi bila ya machafuko, wala kutokuwepo masuala ya ufisadi.
Aidha Askofu Mombeki alimeviomba baadhi ya vyama vya siasa, kuacha tabia ya kusimika wagombea wasio nasifa, ambao hawakubaliki kwa wananchi na matokeo yake kupitishwa kwa nguvu na mamlaka za uchaguzi, hali ambayo imekuwa ikisababisha uvunjifu wa amani nchini.