Jumatano , 7th Jun , 2023

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetoa matumaini mapya kwa wagonjwa wa tezi dume nchini baada ya kuotesha miche ya tiba ya asili kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.

Miche ya kutibu Tezi Dume

Akizungumza katika shamba la miti la Rongai lililopo, North Kilimanjaro Mhifadhi Msaidizi Fred Ng'wavi amesema uoteshaji huo umefanywa kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti ya Muhimbili (MUHAS)

"Miche tunayozalisha hapa ni ya mbao laini, na miche ya miti migumu kutoka kwenye misitu yetu ya hifadhi, tulipo tupo katika kitalu cha miti inayoitwa Brunos Africana ambayo inajulikana kama Mkoma Oyee, ni miti tiba ambayo inatibu tezi dume na taasisi ya utafiti ya Muhimbili (MUHAS) waliingia makubaliano na TFS kwa ajili ya kuzalisha hii miche," amesema Ng'wavi.

Aidha Mhifadhi huyo ameongeza kuwa ndani ya miaka mitano miche hiyo maarufu kwa jina la Mkoma Oyee itaweza kuoteshwa katika mashamba mengine ya TFS yenye hali ya hewa kama ya Rongai

Kwa mujibu wa Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kinasema tezi dume ni moja ya tezi la uzazi la kiume ambalo kila mwanaume analo, ambalo Jinsi umri unavyoongezeka tezi dume nalo huongezeka ukubwa ambao unaweza kuwa wa kawaida au saratani.