Alhamisi , 10th Aug , 2023

Maafisa wa Korea Kusini waliwahamisha zaidi ya watu 10,000 na kufunga shule katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko wakati kimbunga Khanun kilipopiga rasi hiyo na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

 

Baada ya kupiga kusini mwa Japan wiki iliyopita, kimbunga  ilitua kwenye pwani ya kusini mashariki siku ya Alhamisi na kilikuwa kikielekea mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul. Khanun pia huenda kikashambulia mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang, na vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa jeshi na chama tawala vimeamriwa kuandaa hatua za kukabiliana na mafuriko na kuokoa mazao.

Nchini Korea Kusini, safari 350 za ndege na njia 410 za treni zilifutwa, na zaidi ya watu 10,000 walihamishwa kwa usalama, wizara ya mambo ya ndani imesema.

Nchi hiyo bado inaendelea kupata nafuu kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwezi uliopita, ambayo ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 40, ikiwa ni pamoja na 14 katika handaki lililofurika.