
Mfumo wa ulinzi, ambao Rais Donald Trump anapanga kuuzindua mwishoni mwa muhula wake, unalenga kukabiliana na vitisho vya angani vya "kizazi kijacho" kwa Marekani, ikiwa ni pamoja na makombora ya balestiki na cruise.
Wizara ya mambo ya nje ya Pyongyang ilishutumu mpango huo kama kujihesabia haki na kiburi, vyombo vya habari vya serikali viliripoti.
Ilishutumu Washington kwa "kudhamiria... kufanya shughuli za kijeshi katika anga za juu na kuonya kwamba mpango huo unaweza kuibua mashindano ya kimataifa ya silaha za nyuklia na anga.
Korea Kaskazini inaiona Washington kama adui na mara kwa mara imelaani mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini.
Pyongyang pengine inaona ngao hiyo kama tishio ambalo linaweza kudhoofisha silaha zake za nyuklia, Hong Min, mchambuzi mkuu katika Taasisi ya Korea ya Umoja wa Kitaifa, ameliambia shirika la habari la AFP.
Mnamo mwaka wa 2022, Kaskazini ilipitisha sheria inayojitangaza kuwa taifa la silaha za nyuklia, na imejaribu aina mbalimbali za makombora ya balestiki na cruise katika miaka ya hivi karibuni.