Jumatatu , 5th Jan , 2015

Vurugu kubwa imeibuka kati ya askari Polisi na wachimbaji wadogo wakigombea madini ya dhahabu kilo 15 hali iliyosababisha mabomu ya machozi kutumika katika eneo la mgodi, wilayani Geita.

Vurugu kubwa imeibuka kati ya askari Polisi na wachimbaji wadogo wakigombea madini ya dhahabu kilo 15 hali iliyosababisha mabomu ya machozi kutumika katika eneo la mgodi unaomilikiwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Geita Bw. Philimon Sherutete katika kitongoji cha miyombo kijiji cha Rwamgasa wilayani Geita.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Geita Bw. Joseph Msukuma kasheku amefika kwenye eneo la tukio na kusuruhisha mgogoro huo.

Msukuma amesema kuwa mgodi huo umefungwa kwa muda ili wachimbaji wadogo wapate mikataba ya kuendelea na uchimbaji kutokana na fedha walizolipia huku akiwataka wachimbaji wa kati waondoe magari yao kwenye maeneo hayo ili haki itendeke.

Baadhi ya wachimbaji madini wamelilalamikia jeshi la polisi kwa kushindwa kufuata misingi ya uwajibikaji kwa kupora mali za wananchi na kuwafukuza kwenye maeneo yao waliokodishwa kwa gharama ya shilingi 200,000 baada ya kubainika madini ya dhahabu yapo kwa wingi kwenye maeneo hayo.

Akijibu tuhuma zinazowakabili baadhi ya askari polisi mkoani Geita wanaotuhumiwa kupora madini ya dhahabu kilo 15 kamanda wa polisi mkoa wa Geita Bw. Joseph Konyo amedai kuwa askari wameenda eneo la machimbo kusimamia amani na kwamba madini ya Dhahabu yanayogombaniwa yamekabidhiwa kwa afisa madini wa mkoa ili aweze kuthaminisha kwa ajili ya kutozwa kodi ya serikali kisheria.