Nembo rasmi ya CCM
Akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humprey Polepole amesema ushindi huo ni ishara tosha ya jinsi ambavyo watanzania wana imani na chama hicho, na kwamba kuna siri mbili kubwa zilizokipa chama hicho ushindi.
Siri ya kwanza aliyoitaja Polepole ni MAGEUZI ambapo uamuzi wa CCM kuzaliwa upya na kufanya mageuzi makubwa yanayolenga kukirudisha chama hicho kwa wanachama pamoja na kushughulika na shida na kero za watu umefanya watanzania wakielewe zaidi chama hicho.
Siri ya pili ya ushindi wa chama hicho kwa mujibu wa Polepole ni kazi nzuri ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ambaye tangu apewe dhamana ya kuiongoza Tanzania ametekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi nyingi nyingi alizoahidi ikiwemo ya kupambana na rushwa na ufisadi ikiwa ndiyo kazi ya kwanza aliyoanza nayo.
Polepole ametaja ahadi nyingine ambazo zimekuwa ni kivutio kikubwa na kuwafanya watanzania wakipe ushindi chama hicho ni utoaji wa elimu bure, ujenzi wa viwanda, miundombinu ikiwemo ununuzi wa ndege na zaidi ya yote kuwasikiliza wananchi na kero zao.
"Ushindi mliotupatia umetuimarisha kama chama licha ya hujuma, upotoshwaji mkubwa unaofanywa na vyama visivyokuwa CCM.... kubeza jina na nafasi ya Urais watanzania hawakuyaona hayo" Amesema Polepole
Polepole amesema chama hicho kinaendelea na mageuzi ya kiuongozi ili kukifanya kiweze kurudi kwenye misingi yake kwa kuwa na viongoz waadilifu, na wachapakazi, huku kikiendelea kutoa maelekezo kwa serikali kuhusu kuwatumikia wananchi jambo ambalo anaamini kuwa litafanya watanzania waendelelee kukipenda licha ya kubezwa na vyama visivyo kuwa CCM.
Katika chaguzi hizo, CCM imeshinda kwenye kata 19 kati ya kata 20 nchi nzima pamoja na kushinda ubunge katika jimbo la Dimani Zanzibar