Jumatano , 10th Feb , 2016

Mwenyekiti wa klabu ya Kariobangi Sharks inayocheza ligi ya daraja ya chini nchini Kenya Nicholas Mwendwa ameshinda kiti cha urais wa shirikisho la soka nchini humo (FKF).

Mwendwa mwenye umri wa miaka 37 amepata kura 50 kati ya 77 na kumtupa mwenyekiti wa klabu ya Gor Mahia na wakili mashuhuri jijini Nairobi, Ambrose Rachier aliyepata kura 27.

Uchaguzi huo umefanyika leo katika mkutano mkuu wa shirikisho hilo uliofanyika ukumbi wa ndani wa safaricom, katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi.

Mkutano huo pia umemchagua Petra Doris ambaye alikuwa ni mgombea mwenza wa Mwendwa kuwa makamu wa Rais wa shirikisho hilo baada ya kupata kura 53 na kuwashinda Dan Shikanda na Andrew Amukowa.

Baada ya matokeo kutangazwa, wagombea walioshindwa akiwemo mgombea urais Ambrose Rachier wamekubali na matokeo na kumpongeza Mwendwa kwa kuwa Rais mpya wa shirikisho hilo.

Mwendwa ambaye ni mtaalam wa masuala ya TEHAMA, amesema alitarajia ushindi huo, na kwamba sasa wakenya wote wajue kuwa wana shirikisho jipya na lenye damu changa.

Amesema mkakati wake wa kwanza ni kuanza na soka la vijana, na moja kwa moja ataunda timu ya taifa ya vijana, na pia atakuwa na jukumu la kubadilisha mitazamo ya watu kuhusu namna ya kupata ushindi katika soka.

Mapema kabla ya zoezi la upigaji Kura, Rais aliyemaliza muda wake, Sam Nyamweya alitangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro hiyo.