Jumanne , 20th Oct , 2015

Mahakama kuu kanda ya Dar es salaam leo imeahirisha kesi ya kikatiba kuhusu kutoa tafsiri ya umbali wanaotakiwa kusimama wapiga kura baada ya kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu ili kutoa muda kwa upande wa serikali kuandaa majibu.

Jengo la Mahakama kuu ya Tanzania

Awali katika Kesi hiyo inayoongozwa na jaji Sakieti Kihiyo, Aloysious Mujulizi na Lugano Mwandambo walimtaka wakili wa mpigakura Amy Kibatala, aliyefungua kesi hiyo kubadilisha hati ya mashitaka kutoka kwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na kuielekeza kwa mkurugenzi wa tume ya uchaguzi ambaye ndiye mwangalizi wa masuala yote ya uchaguzi.

Kwa upande wao wadaiwa katika kesi hiyo upande wa serikali ikiongozwa na wakili Obadia Kameya umeiomba mahakama kuipa muda mpaka saa nane mchana hii leo ili waweze kuwasilisha majibu ya maombi ya kesi hiyo.

Katika kesi hiyo namba 37 ya mwaka 2015 inayosimamiwa na wakili Peter Kibatala inaiomba mahakama kutoa tafsiri sahihi ya kifungu cha 104 (1) cha sheria ya taifa ya uchaguzi kuhusu umbali ambao mpiga kura anastahili kukaa kutoka kituo cha kupigia kura.

Jaji Sakieti Kihiyo ambaye ni mwenyekiti wa kesi hiyo ameahirisha kesi hiyo mpaka kesho saa tatu itakaposikilizwa tena.