Alhamisi , 3rd Mar , 2016

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amefanya mazungumzo na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, kando ya Mkutano Mkuu wa 17 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha mahusiano.

Baadhi ya maeneo waliyokubaliana kutilia mkazo katika mahusiano hayo, ni pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo inayounganisha nchi mbili ikiwemo ujenzi wa miundombinu, kukuza biashara na kuzalisha ajira kupitia viwanda.

Rais Uhuru Kenyatta amesema amefurahishwa sana kuona rais Dkt. Magufuli yupo tayari kuhakikisha nchi ya Kenya na Tanzania zinakuwa karibu, na miradi ya maendeleo inaharakishwa.

Kwa upande wake rais Dkt. Magufuli, amesema Tanzania na Kenya zina kila sababu ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara hasa katika ujenzi wa viwanda utakaozalisha ajira kwa kuwa watu wake ni wamoja.

Dkt. Magufuli amebainisha kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinajenga mahusiano na ushirikiano zinalenga kupata manufaa hayo ya kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake.

Kabla ya kukutana na Rais Kenyatta Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambapo viongozi hao wamekubalina kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda huku rais Magufuli akimhakikishia kuwa serikali yake itakamilisha ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa ili kurahisha usafirishaji wa bidhaa na watu.

Kwa upande wake Rais Kagame amempongeza rais Magufuli kwa Uongozi wa bora unaolenga kuimarisha uchumi ikiwemo kuimarisha bandari ya Dar es Salaam ambayo rwanda inaitegemea katika kupokea bidhaa zake.