Jumatatu , 4th Sep , 2023

Rais wa Kenya William Ruto amesema kwamba serikali yake itaondoa viza kwa Waafrika wanaokwenda nchini humo ikiwa na maana ya kwamba raia yeyote wa Kiafrika anayetembea Kenya hatahitaji kuwa na viza.

Rais wa Kenya William Ruto

Hayo ameyabainisha hii leo Septemba 4, 2023, wakati akihutubia kwenye uzinduzi rasmi wa Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi Afrika 2023 katika Ukumbi wa KICC, Nairobi, kiongozi wa nchi alisema.

"Miezi isiyo mbali kutoka sasa, tutaondoa hitaji la visa kwa Waafrika wanaotembelea Kenya, sio haki unapotembelea nyumbani hadi uwe na viza," amesema Rais Ruto

Hatua hiyo ya kufungua mipaka ya Kenya kwa nchi zote za Bara Afrika, inawiana na mikakati ya Afrika Mashariki ambapo raia wa ukanda huu hawahitaji kuwa na visa kuzuru nchi yoyote Afrika Mashariki.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeundwa na mataifa 7, yanayojumuisha; Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda na Tanzania.

Kongamano la Mabadiliko ya Tabianchi Afrika 2023, limehudhuriwa na zaidi ya Maraisi 20 kutoka Barani, na viongozi mashuhuri ulimwenguni, kampuni na mashirika yanayotetea uhifadhi wa mazingira.