Alhamisi , 6th Jan , 2022

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, amejiuzulu wadhifa wake hii leo.

Job Ndugai, Spika wa Bunge aliyejiuzulu

Taarifa ya kujiuzulu kwake ameitoa hii leo Januari 6, 2022, na kusema kwamba tayari ameshamuandikia barua ya kujiuzulu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Daniel Chongolo, na nakala yake kuiwasilisha kwa Katibu wa Bunge, na kuongeza kwamba uamuzi alioufanya ni binafsi na hiari na ameamua hivyo kwa maslahi mapana ya Taifa, serikali na chama chake.

Spika Job Ndugai amechukua hatua hiyo, baada ya video zake kusambaa mitandaoni akikashifu fedha za mkopo zilizochukuliwa na serikali kutoka IMF, kwa kusema kwamba deni la taifa limekuwa kubwa na kwamba ipo siku hii nchi itapigwa mnada.

Mara baada ya kauli hizo licha ya Spika Ndugai kumomba radhi kwa Rais Samia pamoja na Watanzania, Rais Samia alioneshwa kukerwa na kiongozi huyo wa Muhimili wa Bunge kutoa kauli kama hizo.

Katika barua yake Spika Ndugai, amewashukuru wabunge wenzake, serikali, wananchi wa jimboni kwake pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa ushirikiano waliompa wakati akitumikia kiti cha Uspika wa Bunge.

Job Ndugai alianza kutumikia nafasi hiyo Novemba 17, 2015 hadi hii leo alipojiuzulu.